Wednesday, December 4, 2019

Uhakiki wa Fani katika Riwaya ya Joka la Mdimu

Fani katika Riwaya ya Joka la Mdimu
Hakiki fani katika Riwaya ya Joka la Mdimu
MWANDISHI: ABDALLAH J. SAFARI
MCHAPISHAJI: HUDA PUBLISHERS
MWAKA: 2007
UTANGULIZI WA KITABU
Joka la mdimu ni riwaya iliyojengwa kwa visa tofautitofauti vinavojengana kukamilisha masimulizi. Ni riwaya inayosawiri au kuakisi mambo yaliyopita ya nyakati za nyuma ambapo kulikuwa na shida kama vile za mafuta ya petroli, Nguo, vyakula nk. Pamoja na hayo zipo pia dhamira au mawazo ambayo yanasawiri maisha ya Mtanzania wa leo kama vile masuala ya rushwa na uhujumu uchumi.
Kwa upande wa fani ni riwaya ambayo mwandishi amewaumba vyema wahusika wake kwa kuwavika uhalisia vyema, amepanga visa vyake na amejitahidi kutumia lugha yenye mvuto na vionjo vya kisanaa huku akiwaburudisha wasomaji kwa mtindo wa kipekee.
JINA LAKITABU
Jina la kitabu limewekwa katika lugha ya picha, JOKA LA MDIMU ni nyoka anayeishi katika miti ya kijani. Nyoka huyu hupendelea kuishi katika miti ya Minyaa na Midimu inayofanana na rangi yake. Nyoka huyu awapo kwenye miti hiyo si rahisi kumtambua kutokana na rangi yake kufanana sana na miti hiyo. Hivyo ni nyoka hatari sana kwa binadamu.
Mwandishi anatumia taswira ya Joka la Mdimu kufananisha na viongozi ambao ni wananchi wenzetu, wanafanana na sisi, ni ndugu zetu damu yetu. Lakini ni hatari mno kwani hutugeuka na kuwa mafisadi, wala rushwa, hawatimizi majukumu yao, ni walaghai nk. Badala ya kusaidia wananchi wao hujali maslahi yao kwanza na hivyo kusababisha mifumo ya kiuchumi kuendelea kuwa migumu kwa wananchi na kupelekea kuongezeka kwa kiasi kikubwa cha watu walio maskini au hohehahe. Hivyo jina la kitabu linasawiri yaliyomo ndani ya kitabu na katika jamii.
MUUNDO
Riwaya ya Joka la Mdimu imetumia muundo changamani yaani kwa kiasi fulani ametumia rejea au rukia pia ametumia muundo sahili au msago.
Mfano ametumia muundo warejeakatika sura ya Mindule ambapo anaanza kutueleza juu ya habari za Amani dereva wa taxi na adha anazopata kutokana na ukosefu wa mafuta na jinsi anavyoiendesha biashara yake hiyo. Lakini ndani ya sura hiyohiyo anaturudisha nyuma na kuanza kutuelezea namna Amani alivyopata kazi ya udereva Taxi na kutueleza juu ya mmiliki wa Taxi hiyo ambaye ni Shiraz Bhanj. Pia katika sura ya Boko anatueleza juu ya Safari ya Tino kwenda kumuona mwanae mgonjwa uk.73 ila hatuelezi inavyoendelea lakini anarukia kisa kingine cha Brown Kwacha na sura ya Kwale halafu badae anaturudisha nyuma na kuendelea kutuelezea juu ya habari za kuuguliwa kwa Cheche na Tino anapofika kumuona katika sura ya Dakta Makwati. Pia ametumia muundo wa moja kwa moja katika sura zingine kwani ameyapanga matukio yake katika usahili bila kuruka.
Pia mwandishi amegawanya visa na mtukio katika sura kumi ambapo kila sura ameipa jina kwa kutumia majina ya wahusika.
·                     Sura ya kwanza, MINDULE:Hapa mwandishi anatueleza kuhusu habari za Amani dereva Taxi, masaibu anayopata katika kazi yake kutokana na uhaba wa mafuta katika vituo vya mafuta.
·                     Sura ya pili, TINO:Hapa tunaelezwa kuhusu maisha ya Tino na kazi anazofanya ya kuvuta kwama. Tunaambiwa kuhusu hali ngumu ya maisha ya Tino na wakazi wengine wa Sega, hapa tunaelezwa pia kuhusu masuala ya uongozi jinsi ulivyo mbovu na ugawanywaji mbovu wa vyanzo vya uchumi na bidhaa.
·                     Sura ya tatu, JINJA MALONI:Katika sura hii tunaelezwa kuhusu maisha ya Jinja Maloni, hapa anaibua dhamira kama vile za uvamizi, uhalifu na mauaji pia anaendela kutueleza kuhusu hali ngumu ya maisha.
·                     Sura ya nne SEGA:Maisha ya wakazi wa Sega yanaelezewa hapa jinsi yalivyo ya dhiki, pia tunaelezwa kuhusu Tino na mkewe maisha yao yalivyo na familia yao, anaibua dhamira ya mapenzi ya dhati na upendo kwa familia.
·                     Sura ya tano, BOKO:Hapa tunaelezwa kuhusu adha ya usafiri kwa watu, shida ya mafuta, ubovu wa miuondmbinu kama vile barabara, vinasemwa hapa.
·                     Sura ya sita, BROWN KWACHA:Sura hii inaeleza habari za Brown maisha yake na tabia zake, anaibua dhamira kama vile uhujumu uchumi, biashara za magendo, suala la kutowajibika kwa watumishi, suala la kukosekana kwa uaminifu katika ndoa na mapenzi ya pesa ambapo sifa zote hizi alizibeba Kwacha.
·                     Sura ya saba, KWALE:Hapa yanaelezwa mambo kuhusu hifadhi ya Kwale, safari ya Brown na Leila kwenda kutembea kwale. Hapa yanatajwa mambo ya udhalimu wa kuharibu mali za umma (maliasili za taifa) mfano pembe za ndovu, vipusa pia mapenzi yasiyo ya kweli.
·                     Sura ya nane, DAKTA MIKWALA:Dakta Mikwala ndiye mhusika mkuu anayeelezwa hapa, tunalezwa juu ya ugumu wa upatikanaji wa huduma za afya kwani Cheche anashindwa kutibiwa kutokana na ukosefu wa fedha za kigeni.
·                     Sura ya tisa, CHECHE:Tunaelezwa juu ya juhudi za Amani na Tino ili kumsaidia Cheche aweze kwenda kutibiwa Uingereza. Wanafanikiwa kupora benki na kupata pesa za kumtibu Cheche.
·                     Sura ya kumi, MOTO:Hapa hatma ya visa vidogo vidogo imeelezwa kwa kutolewa hatma ya maisha ya Cheche na Brown Kwacha. Cheche alipata matibabu na kupona na Browna anafanikiwa kuirubuni serikali kwa kuipanga mahesabu ya uongo.
MTINDO
Mwandishi ametumia mitindo ya aina tofautitofauti ili kuweza kuipamba kazi yake ivutie.
·                     Matumizi ya nafsi ya tatu Umoja. Imetawala: Mfanouk.5“Amani aliangalia…….” Uk.25 “Amani alijizuia” .Nafsi ya tatuwingi;mfano uk. 63“ wote walitoka nje kuelekea klabuni”.Piauk.53 “wale wanaume walimvamia”
·                     Matumizi ya nafsi ya pili: Mfanouk.106 “ mmechoka kuangalia video?” “aa tumeshaziona mara nyingi tunaombaainanyingine.” Mazungumzo baina ya mke wa Brown na wanae.Pia mazungumzo baina ya Brown na Leila.Uk.113. “habari za asubuhi”“ Nzuri sijui wewe” alijibu“Uliota njozi njema?”"Wapi?""Kwa nini?"
·                     Matumizi ya nafsi ya kwanza: Mfanouk. 39 “mimi nimemaliza” “….kuiba nimeiba sana….”
·                     Matumizi ya nyimbo.Uk.70. wimbo wa Chaupele: “Chaupele mpenzi, haya usemayoKama ni maradhi, yapeleke kwa DaktariWanambia niache rumba,na mimi sikuzoeaSitaweza kuliacha rumba, kwa sababu yakoKama wanipenda, nenda kwa baba”Piauk.58 “sega! Sega! Sega!, usioogope” wimbo waliouimba washabiki wa michezo.
·                     Masimulizi ya hadithi ndani ya hadithi: Hapa mwandishi amemtumia muhusika kusimulia kisa kingine kidogo ndani ya kisa kikuu. Mfanouk.39mhusika Tino anamsimulia mteja wake maisha yake ya mwanzo kabla hajaanza kazi ya kuvuta kwama.
MATUMIZI YA LUGHA
Mwandishi A. Safari ametumia lugha fasaha na inayoeleweka kwa wasomaji wake. Kuna matumizi ya lugha nyinginezo kama vile kiingereza.Uk.55 “city devils” uk.155 “I miss my family”, uk.24 “Hey man you will pay extra money”, uk.99 consignment”.Pia kuna matumizi ya lugha ya kiarabu, mfanouk.45 “Salaam aleikum mayitun” uk.42 “Inna Ilayhi Raajiunna!”, uk.13, “Insha Allah!”. Vilevile kuna matumizi ya lugha ya mtaaniuk.39 “msela”, “ndito”, “kashkash”.
Matumizi ya tamathali za semi.
·                     Tashibiha:Uk.117 “ngozi yake nyeusi kama udongo wa mfinyanzi”Uk.122 “mweusi kama sizi la chungu”Uk.9 “Zepher 6 ile iliunguruma kama simba dume”Uk.10 “mteuzi mithili ya Mbega”Uk.35 “……miguu yake ikakazana mithili ya upinde uliotaka kufyatuliwa”
·                     Sitiari:Uk.91 “Brown Kwacha alikuwa kinyonga”Uk.15 “sarahange wetu mboga kweli siku hizi”Uk.40 “huku twakaa vinyama vya mwitu”Uk.72 “sote ni kobe”
·                     Tashihisi:Uk.109 “……gari lile zuri lilioondoka kwa madaha” Uk.143 “ kuta nyeusi za nyumba zaidi ya kumi zilisimama twe!kuomboleza” Uk.91 “pua zake zikalakiwa na riha na ashrafu ya manukato”;Uk.12 “utumbo ulimlaumu”; Uk.27 “mvua ikapiga kwa kiburi na kuviadhibu vibati vibovu”.
·                     Tafsida:Uk. 49 “isijekuwa nimekukatiza haja!”,piauk.hohuo“kinyesi”.
Mbinu nyingine za kisanaa.
·                     Takriri:Uk.151 “mwizi! Mwizi! Jambazi! Jambazi!”Uk.57 “shinda! Shinda! Shinda!”Uk.33 “karibu baba, kariibu kaka, karibu mkwe” Uk.72 “uhuru upi? Uhuru gani? Uhuru wa nini na nani?”
·                     Mdokezo:Uk.149 “lakini……..”
·                     Onomatopea au tanakali sauti:Uk. 1 “saa mezani niliendelea kugonga taratibu ta! ta! ta!”; Uk.10 “ikatoka sauti kali tupu ta nye nye”;Uk.67 “upepo wa stova uliolia shshsh”;
·                     Tashtiti:Uk.113. leila anamuuliza Brown maswali ambayo anayajua majibu yake. Brown:“uliota njozi njema? Leila: Wapi?” Leila:Kwanini? Brown:Mwenywe unajua”
·                     Nidaa:Uk.39 “Aaa! Limbukeni wa jiji anataka kunitia kashkash”: Uk 30 “nguo zangu Mungu wee!” Uk.42 “Inna Lillah wa Inna Ilayhi Raajiunna!” Uk.92 “Ah! Leila kwacha alimsalimia kwa furaha” Uk. 105 “Lahaula”
Matumizi ya Semi.
·                     Methali:Uk.78 “asilojua mtu ni usiku wa kiza”Uk.83 “ukiona mwenzako anyolewa zako tia maji”Uk.98 “mtaka waridi sharti avumilie miiba”Uk. 99 “biashara haigombi”Uk.43 “ajizi nuksani huzaa mwana kisirani”
·                     Misemo:Uk.10 “asiye na bahati habahatishi”Uk.47. “asiyezika hazikwi”Uk.64 “mmetupa Jongoo na mtiwe”Uk.98 “asali haichomvwi umoja”Uk.111 “ajali haina kinga”Uk.115 “mwenye macho haambiwi tazama”Uk.120 “matendo hushinda maneno”Uk.47. “asiyezika hazikwi”
·                     Nahau:Uk.11 “sio unanilalia kila mara” –kunidhulumuUk.107 “alikonda akajipa moyo” –kujifariji moyo
Matumizi ya taswira
Taswira mwonekano imetumika, ambayo inatujengea picha kutokana na vitu tunavyovifahamu. Mfanouk.76 “alisema kijana mmoja wa kiume kavaa sketi, blauzi na sidiria iliyopachikwa juu yake. Kichwani alifunga kilemba.”Hii inatupa picha halisi ya huyo kaka kwani tunaposoma ni kama kweli tunamuona kutokana na jinsi mwandishi alivyoelezea. Piauk.135 “mwambie yule jamaa pale atayarishe kuku mzuri wa kukaanga”……… na kachumbari yenye pilipili”hii inamfanya msomaji ahisi ladha ya kuku na hiyo pilipili kwa maneno ambayo mwandishi ameyajengea taswira na hii ni taswira hisi.
Joka lamdimuni taswira ya nyoka mbaya ambaye amefananishwa na viongozi wabaya.
WAHUSIKA
AMANI
·                     Ni dereva taxi
·                     Ana upendo wa dhati
·                     Ni mchapakazi
·                     Ana hekima na busara
·                     Ana huruma
·                     Ni rafiki wa kweli wa Tino
·                     Kutokana na hizo sifa amani ni mhusika bapa
·                     Anafaa kuigwa na jamii
TINO (mhusikabapa)
·                     Ni mchapakzi
·                     Mlezi bora wa familia
·                     Baba wa Cheche
·                     Ana huruma
·                     Ana upendo wa dhati
·                     Ni makini
·                     Ni jasiri
·                     Ni mwanamichezo
·                     Anafaa kuigwa na jamii
BROWN KWACHA
·                     Ni mkurugenzi wa idara ya fedha za kigeni
·                     Ni muhuni na Malaya
·                     Fisadi na mla rushwa
·                     Anafanya biashara haramu
·                     Hana mapenzi kwa familia yake
·                     Anapenda anasa
·                     Si muaminifu kwa mkewe
·                     Si muadilifu
·                     Hafai kuigwa na jamii
·                     Ni mhusika bapa
JINJA MALONI
·                     Ni jasiri na mwenye nguvu
·                     Ana huruma na upendo
·                     Mchapakzi
·                     Mlevi
·                     Maskini
·                     Ni mhusika duara
DAKTARI MIKWALA
·                     Ni daktari bingwa wa mifupa
·                     Anapenda rushwa
·                     Si muwajibikaji katika kazi yake
·                     Ni mlevi
·                     Hafai kuigwa na jamii
·                     Ni mhusika bapa
SHIRAZ BHANJ
·                     Ni mfanyabiashara
·                     Ni mtoa rushwa
·                     Ana biashara za magendo
·                     Rafiki wa Brown
·                     Hafai kuigwa na jamii
·                     Ni mhusika bapa
ZITTO
·                     Ni mfanyakazi bandarini
·                     Ni mwanamichezo
·                     Ni jasiri ana kipato duni
·                     Rafiki wa Tino na Aman
CHECHE
·                     Ni mtoto wa Tino
·                     Ana nidhamu na bidii
·                     Ni mwanamichezo
·                     Ana upendo kwa wazazi wake
·                     Ni mtiifu na msikivu
·                     Mcheshi na mudadisi
·                     Alivunjika kiuno michezoni
·                     Ni mhusika bapa
MWEMA
·                     Ni mke wa Tino
·                     Mvumilivu
·                     Ana mapendo ya dhati kwa familia yake
·                     Ni mchapakazi
·                     Ni mhusika bapa
JOSEPHINE NA LEILA
·                     Wasichana wahuni waliojiuza kwa Brown Kwacha
·                     Hawafai kuigwa na jamii
MANDHARI

Mandhari aliyoitumia mwandishi ni ya mjini, anataja baadhi ya maeneo ya nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam kama vile Boko, Sega, Mindule. Mandhari hii ni sadifu kwa yale ambayo mwandishi ameyaeleza kwani masuala ya rushwa, upotevu wa haki, hali ngumu ya uchumi na maisha kwa ujumla, ni matatizo halisi ya jamii ya Tanzania.

No comments:

Post a Comment

CHUO CHA UALIMU MONTESSORI-MTWARA

Uhakiki Fani katika Ushairi wa Malenga Wapya

Fani katika Ushairi wa Malenga Wapya Hakiki Fani katika Ushairi wa Malenga Wapya MWANDISHI: TAASISI YA KISWAHILI, ZANZIBAR WACHAPISHA...