UKUAJI
NA UENEAJI WA KISWAHILI ENZI YA WAINGEREZA NA BAADA YA UHURU
kuna mambo waliyofanya waingereza yaliyosaidia
kukua na kuenea kwa Kiswahili, mambo hayo ni kama yafuatayo:
Shuguli za kiuchumi
Shuguli za kiuchumi wakati wa Waingereza zilihusisha kilimo na
biashara. Kwa upande wa klimo, Waingereza waliendesha kilimo cha mazao
mbalimbali, na walitumia mfumo wa kuajiri vibarua kutoka sehemu mbalimbali za
nchi. Vibarua hao walijulikana kwa jina la manamba.
Katika mkusanyiko wa vibarua hawa waliokuwa na usuli wa makabila
tofautitofauti, lugha pekee iliyoweza kuwaunganisha ni Kiswahili ikizingatiwa
kwamba Kiswahili kiliteuliwa kuwa lugha rasimi katika mawasiliano ya kiutawala.
Walilazimika kuzungumza Kiswahili kwani bila hivyo mawasiliano yasingeweza
kufanyika kwa urahisi.
Hata hivyo kupitia shuguli za kilimo maneno mapya ya Kiswahili
yaliweza kuzaliwa, kwa mfano: yadi, belo, belingi, bani, mtama n.k, kwa hiyo
kupitia shughuli hizi Kiswahili kilizidi kukua.
Shuguli za kiutamaduni
Shughuli hizi ni kama vile uigizaji wa tamthiliya za kigeni,
uchezaji wa mziki wa kigeni hususani twisti. Tamthiliya za kigeni zilikuwa
zikiigizwa majukwaani kwa lugha ya Kiswahili na hivyo ikasaidia kukua kwa
msamiati wa Kiswahili.
Shughuli za kidini
Wakati wa utawala wa mwingereza pia kuliambatana na ujio wa
wamishonari waliokuwa na lengo la kueneza dini ya kikristo.
Katika harakati hizi walitumia lugha ya Kiswahili ili
kufanikisha malengo yao ikizingatiwa kwamba Kiswahili kilikuwa kimeshaenea vya
kutosha wakati wa utawala wa Mjerumani, kwa hiyo wamishonari wa Kiingereza
waliendelea kukiimarisha zaidi.
Pia shughuli za kidini zilipelekea kutafsiriwa kwa vitabu
mbalimbali vya kidini kama vile Biblia na vitabu vingine. Tafsiri ya vitabu
hivi ilikuwa ni kutoka katika lugha ya kiingereza kwenda katika lugha ya
Kiswahili. kwa kufanya hivi Kiswahili kiliweza kuingiza msamiati mwingi sana na
hivyo kukuza lugha ya Kiswahili.
Wamishonari walilazimika kujifunza Kiswahili hukohuko kwao ili
wanapokuja huku Afrika Mashariki wasipate tabu ya kujifunza Kiswahili. Kwa
sababu hii wamishonari waliokuwa wamekwishajifunza lugha ya Kiswahili walitunga
kamusi za Kiswahili – Kiingereza ili kuwasaidia wenzao pia kujifunza Kiswahili;
kwa njia hii waliweza kukikuza Kiswahili.
Shughuli za kisiasa
Shughuli za kisiasa hasa katika uanzishwaji wa vyombo mbalimbali
vya kiutawala, jeshi, polisi, mahakama, boma n.k. Kufuatia uanzishwaji wa
vyombo hivi msamiati mwingi wa Kiswahili uliweza kuzuka na hivyo kukuza
Kiswahili.
Shughuli za kiutawala
Makampuni ya uchapishaji yalianzishwa (East African literature
Bureau), na kamati ya lugha iliundwa (Interterritorian language committee).
Hatua hii iliimarisha matumizi ya lugha ya Kiswahili hali iliyosaidia kukua kwa
lugha ya Kiswahili.
Shuguli za ujenzi wa reli na barabara
Shughuli hizi pia zilisaidia kuibuka kwa msamiati mpya kama
vile, reli, stesheni, tiketi
n.k.
Usanifishaji wa Kiswahili
Usanifishaji wa lugha ya Kiswahili pia lilikua ni jambo jingine
muhimu sana lililosaidia kukua kwa msamiati wa Kiswahili. Lengo la usanifishaji
wa Kiswahili lilikuwa ni kuleta ulinganifu wa matumizi ya lugha ya Kiswahili
katika ukanda wa Afrika Mashariki.
UENEAJI WA KISWAHILI
Ukuaji na Ueneaji ni maneno mawili yenye maana zinazokaribiana
lakini zinazotofautiana. Ukuaji humaanisha ongezeko la msamiati katika lugha na
ueneaji ni uongezekaji wa matumizi ya lugha kieneo. Kwa hiyo hapa tutaangalia
yale mambo yaliyosababisha Kiswahili kitumike katika eneo kubwa. Mambo hayo ni
haya yafuatayo:
Vyombo vya habari
Vyombo vya habari vilivyokuwepo kwa wakati huo ni redio,
magazeti na majarida mbalimbali. Kwa upande wa redio kulikuwepo na redio
Tanganyika iliyoanza kurusha matangazo yake kwa kutumia lugha ya Kiswahili. Na
magazeti yaliyokuwa yakichapishwa wakati huo ni pamoja na: Mambo leo, Sauti ya
Pwani, Kiongozi na Habari za leo. Magazeti haya yote yalikuwa yakichapishwa kwa
lugha ya Kiswahili. Kwa hiyo kwa kutumia vyombo vya habari (redio na magazeti)
kiswahili kiliweza kuenea.
Kilimo
Kupitia kilimo watu waliweza kukutana pamoja, watu wa makabila
tofautitofauti. Kwa hiyo katika kipindi chote walichokaa kwenye makambi ya
mashambani waliweza kujifunza Kiswahili na walipomaliza muda wao walirudi
nyumbani wakiwa wamejifunza lugha mpya na hivo kwa njia hii waliweza kuieneza
lugha ya Kiswahili.
Muundo wa jeshi la
kikoloni (KAR)
Jeshi la KAR liliundwa na watu kutoka makabila mablimbali, na
lugha iliyokuwa ikitumika jeshini ni Kiswahili, askari hawa walisaidia kueneza
lugha ya Kiswahili ndani na nje ya nchi kwani kila walipokwenda walikuwa wakizungumza
Kiswahili.
Mfumo wa elimu
Chini ya utawala wa Waingereza Kiswahili kilitumika katika
masomo yote kwa ngazi ya shule ya msingi, na pia kilitumika kama somo kwa ngazi
ya shule za sekondari. Kwa hiyo hii pia ilichangia kuenea kwa lugha ya Kiswahili
Harakati za kudai uhuru
Chama cha TANU kilianzisha harakati za kudai uhuru, harakati
hizo ziliendeshwa kwa lugha ya Kiswahili. Kwa hiyo kupitia harakati hizo
Kiswahili kiliweza kuenea kwa kiwango kikubwa.
Tathimini ya maendeleo ya Kiswahili wakati wa Waingereza
Licha ya maendeleo ya lugha ya Kiswahili katika utawala wa
Waingereza, pia kulikuwa na changamoto zilizoikabili lugha ya Kiswahili katika
kupiga hatua ya maendeleo. Changamoto hizo ni kama zifuatazo:
Kutofundishwa kwa
Kiswahili shule zote nchini
Wakati wa utawala wa Waingereza Kiswahili kilifundishwa katika
shule za watoto wa kiafrika tu, wakati katika shule za watoto wa kizungu
Kiswahili hakikufundishwa. Kwa hiyo suala hili lilifanya Kiswahili kipewe
msukumo mdogo sana na hivyo kuhafifisha ukuaji wake.
Kutotumika kwa Kiswahili
kama lugha ya kufundishia
Lugha ya Kiswahili ilitumika kufundishia katika shule za msingi
pekee ilihali lugha ya kiingereza ilitumika kuanzia shule za sekondari hadi
elimu ya juu. Hali hii ilisababisha watu kujitahidi sana kujifunza kiingereza;
kwa kuzungumza kiingereza ilikuwa na ishara kwamba wewe ni msomi, na hivyo
kutokana na hali hii Kiswahili kilendelea kukua polepole sana.
Kukosekana kwa vyombo vya
kizalendo vya kukuza Kiswahili
Vyombo vilivyokuwa vinahusika na masuala ya ukuzaji wa Kiswahili
wakati wa ukoloni vilikuwa vimeanzishwa na wakoloni wenyewe, kwa mfano Kamati
ya Lugha ya Afrika Mashariki (Inter-Territorial Swahili Language commitee) na
Shirika la maandiko la Afrika Mashariki (East African Literature Bureau). Katika
hali kama hii ukuzaji wa Kiswahili ulikosa msukumo mkubwa wa kizalendo.
Kasumba ya kuthamini
Kiingereza
Wananchi walikuwa na kasumba kwamba mtu anayezungumza Kiingereza
alichukuliwa kuwa ni mtu mwenye maendeleo na msomi, kwa hiyo hali hii
ikapelekea watu kutothamini Kiswahili na hivyo Kiswahili kudharaulika.
Ukuaji na Ueneaji wa Kiswahili baada ya
Uhuru
Shughuli
mbalimbali zinazowezesha Kukua na Kuenea kwa Kiswahili nchini
Elezea shughuli mbalimbali zinazowezesha kukua na kuenea kwa
Kiswahili nchini
Baada ya uhuru kuna harakati mbalimbali zilizochukuliwa na
serikali ya Tanzania katika kukiendeleza na kukikuza kiswahili. Harakati hizo
ni pamoja na kupendekezwa kuwa lugha rasmi 1962. Mkwaka 1964 kiswahili
kilipendekezwa kuwa lugha ya taifa na kuwa kitatumika katika shughuli zote za
kiserikali na kitaifa mfano katika elimu hususani elimu ya msingi.
Kuundwa kwa Chombo cha usanifishaji ambacho kilikuwa na kazi ya
kuhimiza maendeleo ya kiswahili, kutayarisha kamusi na vitabu mbalimbali vya
sarufi na fasihi ya lugha ya kiswahili na kuandaa wataalamu watakaoshughulikia
usanifishaji wa Kiswahili
Pia baada ya uhuru kulianzishwa Taasisi mbalimbali
zitakazoshughulikia lugha ya kiswahili. Mfano:- BAKITA, TUKI, TUMI, UKUTA,
UWAVITA, Idara ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaamu.
Baada ya uhuru nchini Tanzania kiswahili kilienea kwa kasi kubwa
sana. Kuna sababu mbalimbali ambazo zilichangia kukua na kuenea kwa kiswahili
hapa nchini. Baadhi ya sababu hizo ni pamoja na kuteuliwa kwa kiswahili kuwa
lugha ya Taifa, Kiswahili kitumike katika Elimu, mfano kuwa lugha ya
kufundishia katika shule za msingi. Kuundwa kwa vyombo mbalimbali vya kukuza na
kuneza kiswahili, Kiswahili kuwa Lugha rasmi na lugha ya Taifa, shughuli
mbalimbali za kidini, shughuli za kisiasa na kiutawala na shughuli za
kiutamaduni na uchapishaji wa vitabu na majarida mbalimbali.
Kiswahili kuwa lugha ya taifa
Baada ya uhuru mwaka 1962 kamati iliundwa ili kuangalia
uwezekano wa kutumia kiswahili katika shughuli zote rasmi, mfano bungeni na
shughuli zote za kiofisi. Pia kiswahili kiliteuliwa kuwa lugha ya taifa 1964
ambapo katika shughuli zote za kitaifa zitaendeshwa kwa kutumia lugha ya
kiswahili. Hivyo kiswahili kilihimizwa kutumika katika mawasiliano yote hasa
katika shughuli za umma na Wizara zote, Serikali na Bunge, kiswahili
kiliendelea kupanda hadhi zaidi wakati wa Azimio la Arusha la mwaka 1967 kwani
azimio hilo lilitungwa na kuandikwa kwa lugha ya kiswahili.
Kuundwa kwa vyombo vya ukuzaji na uenezaji wa Kiswahili
Tanzania baada ya uhuru ilifanya jitihada za kuunda vyombo
mbalimbali vya kukuza na kueneza Kiswahili katika nyanja mbalimbali mfano wa
vyombo hivyo ni UWAVITA BAKITA, TUKI, Taasisi ya Elimu,TAKILUKI na Chama cha
Kiswahili Chuo Kikuu Dar es Salaam.
Kutumika katika elimu
Kiswahili licha ya kutumika katika shughuli mbalimbali za
kiserikali, kilipendekezwa kutumika katika shule za Msingi na kufundishwa
katika elimu ya sekondari kama somo na katika vyuo vikuu wanatoa shahada
mbalimbali za lugha ya kiswahili. Pia katika Elimu ya watu wazima ambao
hawakujua kusoma na kuandika. Watu hawa walijifunza masomo mbalimbali kwa lugha
ya kiswahili na kuwafanya watu wengi kujua kusoma, kuandika na kuzungumza lugha
ya kiswahili fasaha. Kampeni hii ilikuwa kwa nchi nzima ambapo walijifunza
elimu ya Afya, Siasa, Kiswahili, Kilimo na ufundi kwa lugha ya Kiswahili na
kuwafanya watu wengi kuzungumza kiswahili sanifu.
Vyombo vya habari
Tangu uhuru ulipopatikana kuna vyombo mbalimbali vya habari
vilivyoanzishwa. Vyombo hivi hutumika kueneza kiswahili kwa kiasi kikubwa na
hufikiwa na watu wengi licha ya kuwepo kwa changamoto za kiuchumi. Vyombo hivyo
ni magazeti na majarida mbalimbali ambayo huandikwa kwa lugha ya kiswahili
lakini kuna redio na runinga ambazo matangazo yake hutangazwa kwa lugha ya
kiswahili. Hivyo kukifanya kiswahili kuenea kote ndani na nje ya nchi.
Biashara
Shughuli za kibiashara nchini husaidia kuenea na kukua kwa
kiswahili kutokana na kuwepo kwa makabila tofauti tofauti ambapo
wafanyabiashara huweza kuunganishwa kwa lugha ya kiswahili. Hivyo kiswahili
hudumishwa na kutumika katika biashara hizo.
Shughuli za siasa na utawala
Tangu wakati wa harakati za kupigania uhuru kiswahili kimetumika
kama nyenzo muhimu kuwaunganisha wananchi. Shughuli za kisiasa zimetumia lugha
hii katika kujiimarisha; mfano wakati wa chama kimoja, Azimio la Arusha na
Mfumo wa vyama vingi Kiswahili kimetumika kama njia kuu ya mawasiliano. Pia
katika utawala chama kinachotawala kimekuwa na harakati za kukiendeleza
kiswahilli katika nyanja zote. Ambapo kiswahili kimekuwa kikitumika katika
shughuli zote za kiutawala. Hivyo shughuli za kisiasa na kiutawala zimechangia
kwa kiasi kikubwa katika kukuza, kukieneza na kukiendeleza kiswahili.
Uandishi na uchapishaji wa vitabu
Kuibuka kwa waandishi wa vitabu mbalimbali vya kiswahili vya
sarufi na fasihi ambavyo vilichambua kwa kina mambo mabalimbali yahusuyo lugha
ya kiswahili na utamaduni wake, mfano :- F Nkwera, Shabani Robart, Mathias
Mnyapala na Shaffi Adam Shaffi. Waandishi wengine chipukizi walijitokeza na
wanaendelea kujitokeza katika tasnia hii ya uandishi wa vitabu.
Shughuli za kiutamaduni
Shughuli za kiutamaduni zimechangia kueneza kukuza na kuendeleza
lugha ya Kiswahili. Shughuli hizo ni pamoja na harusi, misiba, matanga na
sherehe mbalimbali za kijamii ambazo zimesaidia kukiendeleza Kiswahili kwa kuwa
huwakutanisha watu tofautitofauti katika shughuli hizo, ambapo huwalazimu
kutumia lugha ya kiswahili katika mawasiliano na kufanya kiswahili kuendelea.
Pia katika Sherehe mbalimbali vikundi vya sanaa na muziki vinavyotumia lugha ya
kiswahili kutumbuiza. Vikundi vingine huandaa nyimbo zao kwa ajili ya kukieneza
Kiswahili.
Vyombo vya Ukuzaji na Uenezaji wa Lugha ya Kiswahili
Tangu Tanzania ipate uhuru hadi sasa kuna vyombo kadha wa kadha
vilivyoanzishwa kwa ajili ya kukuza na kueneza Kiswahili baadhi ya vyombo hivyo
ni hivi vifuatavyo:
BAKITA
Hii ni taasisi ya serikali iliyoundwa kwa sheria ya Bunge Na.27
ya mwaka 1967 kwa madhumuni ya kukuza Kiswahili. Kutokana na sheria hii Baraza
ndilo mratibu wa kusimamia asasi zote na mawakala wote wanaokuza Kiswahili
katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
BAKITA imekuwa na mchango mkubwa sana katika ukuzaji na uenezaji
wa lugha ya Kiswahili kupitia majukumu yake. Majukumu ya Baraza kama
yalivyofafanuliwa katika sheria hiyo ni haya yfuatayo:
·
Kuratibu
na kusimamia maendeleo na matumizi ya Kiswahili nchini kote.
Katika kufanya hivi Baraza lina jukumu la kuhakikisha Kiswahili kinaendelea na
kuhakikisha kuwa matumizi ya Kiswahili yanakuwa sahihi.
·
Kushirikiana
na vyombo vingine nchini vinavyojihusisha na maendeleo ya Kiswahili na kuratibu
shughuli zao. Vyama vya Kiswahili kama vile CHAKAMA,
CHAWAKAMA vina mchango mkubwa wa kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili kwa
kushirikiana na BAKITA. Ushirikiano wa BAKITA na vyama hivi waweza kuwa ni wa
kuto ushauri, au msaada wa kifedha, kwa mfano BAKITA imekuwa ikiwasaidia
CHAWAKAMA pale wanapokuwa wanataka kufanya makongamano nap engine wanahitaji
msaada wa kifedha, kwa hiyo BAKITA imekuwa ikiwasaidia kifedha.
·
Kuhimiza
matumizi ya Kiswahili katika shughuli rasmi na za kawaida. BAKITA
imekuwa ikiandaa vipindi mbalimbli redioni ili kuhimiza matumizi sahihi ya
lugha ya Kiswahili.
·
Kushirikiana
na mamlaka zinazohusika kuthibitisha tafsiri sanifu za istilahi. Katiaka
uundaji wa istilahi, BAKITA imekuwa ikichapisha vitabu mbalimbali ikionesha
istilahi sanifu zilizoingizwa katika lugha ya Kiswahili. kwa hiyo kupitia
jukumu hili Kiswahili kimekuwa kinakua.
·
Kutoa
huduma za tafsiri na ukalimani kwa serikali, mashirika ya serikali na yasiyo
yaserikali na asasi nyingine. Kupitia tafsiri
zinazofanywa na BAKITA Kiswahili kimekuwa kikikuwa na kuenea.
·
Kuchapisha
jarida au toleo linalohusu lugha na fasihi ya Kiswahili. Machapisho
haya ya BAKITA yanaendelea kukifanya Kiswahili kukua kwa kuongeza msamiati mpya
na hivyo watu wanaposoma machapisho hayo wanajifunza msamiati mpya na hivyo
kufanya Kiswahili kukua.
·
Kushirikiana na mashirika
ya kitaifa, asasi na watu binafsi, kufuatilia, kushauri na kusimamia shughuli
zinazolenga kukuza Kiswahili nchini Tanzania.
·
Kutoa
ushauri kwa waandishi na wachapishaji ili watumie Kiswahili fasaha. Kwa
kufanya hivi matumizi bora ya Kiswahili yanakuwa yanaimarika.
·
Kushirikiana
na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuthibitisha vitabu vya Kiswahili
vitakavyotumika shuleni na vyuoni kabla havijachapishwa. Hili
pia ni jamabo linaloimarisha matumizi ya Kiswahili sanifu.
TAKILUKI
Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni (TAKILUKI) ilianzishwa
mwaka 1979 kwa lengo la kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya
Zanzibar, ili kutimiza lengo hilo TAKILUKI inajishughulisha na kazi zifuatazo:
·
Kuratibu na kuendesha
mafunzo ya lugha ya Kiswahili visiwani Zanzibar, kuendesha mafunzo ya lugha ya
Kiswahili kwa wazawa na wageni, kuhariri miswada mbalimbali ili kuthibitisha
ufasaha wa Kiswahili na kufanya tafiti za Kiswahili katika Nyanja zake zote,
hususani katika uwanja wa sarufi na fasihi.
·
Pia TAKILUKI wana kazi ya
kuandaa istilahi za taaluma mbalimbali, kutoa huduma za taaluma mbalimbali,
kutoa huduma za tafsiri na ukalimani kwa lugha mabalimbali kwa mashirika,
idara, wizara, taasisi, kampuni na watu binafsi, kufundisha lugha za kigeni na
kuandika vitabu mbalimbali vya Kiswahili.
·
Pia hujishughulisha na
utoaji wa ushauri wa kitaaluma kwa watunzi wa vitabu ili waweze kuandika kazi
zenye ubora, na kushirikiana na wadau wengine wa Kiswahili kama vile,
mashirika, wizara, taasisi, vyuo na watu binafsi katika kuendesha shuguli za
ukuzaji wa Kiswahili, mathalani kuandaa na kuendesha semina, warsha na kozi
fupifupi za Kiswahili.
·
Vilevile hujishugulisha
na usimamizi na ufuatiliaji wa matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili katika
vyombo vya habari na katika shughuli mbalimbali za serikali na za kawaida.
TUKI/TATAKI
Majukumu ya TUKI ni pamoja na kuunda sera muafaka za kustawisha
Kiswahili na pia kufanya utafiti katika lugha ya Kiswahili.
Majukumu mengine ya TUKI ni kuhariri, kuchapisha vitabu na
kutawanya vitabu na majarida ya kitaaluma katika Kiswahili.
Kwa sasa TATAKI inatoa shahada ya awali na uzamili katika lugha
ya Kiswahili, kwa njia hii inawaandaa wataalamu wa lugha ya Kiswahili ambao
watatumika sehemu mbalimbali za ulimwengu kufundisha lugha ya Kiswahili.
CHAUKIDU
CHAUKIDU ni kifupi cha Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani,
makao makuu ya chama hiki kwa sasa yapo chuo kikuu cha Wisconsin-Madison,
Marekani
Madhumuni makuu ya CHAUKIDU ni: Kuwajumuisha pamoja wakuzaji wa
Kiswahili duniani kote kwa lengo la kuchochea kasi ya malengo mahususi
yafuatayo:
·
Kukuza
Kiswahili katika nyanja zote ambamo lugha hii inatumika au inaweza
kutumika na kuongeza ufanisi wa mawasiliano katika ufundishaji na utafiti wa
maarifa ya aina zote, uandishi/utangazaji wa habari, uandishi wa vitabu,
uchapishaji vitabu na majarida, utayarishaji wa safari za mafunzo katika Afrika
ya Mashariki na Kati, n.k.
·
Kusambaza
habari na matokeo ya utafiti kwa kutumia
machapisho mbalimbali na teknolojia ya mtandao wa kompyuta juu ya vipengele
mbalimbali vya Kiswahili na masuala yanayohusiana na Kiswahili.
·
Kuwajumuisha
wanachama kwa ajili ya kubadilishana mawazo na tajiriba zao katika
masuala mbalimbali yanayohusu Kiswahili (k.v. uboreshaji wa ufundishaji,
utangazaji, utafiti, uandishi, nk.) kwa njia ya mkutano wa kila mwaka, warsha
au semina au kongamano maalumu, na hata kwa njia ya mtandao.
·
Kuelimisha
umma juu ya umuhimu wa kujivunia, kuendeleza, na kuheshimu
Kiswahili.
·
Kushauri
ama kushinikiza serikali za nchi ambamo Kiswahili
kinazungumzwa kutambua thamani iliyobebwa na maliasili hii ili kuunda sera
muafaka za kukiendeleza kadri ya uwezo wake kwa manufaa ya maendeleo ya
serikali na watu wake kijamii, kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni, kielimu, n.k.
CHAWAKAMA
CHAWAKAMA husimama badala ya Chama cha Wanafunzi wa Kiswahili
vyuo vikuu Afrika Mashariki. Chama hiki kilianzishwa mwaka 2004 kwa lengo la
kukuza na kueneza Kiswahili katika eneo lote la Afrika Mashariki kupitia
wanafunzi wanaosoma Kiswahili vyuoni. Wanachama wa chama hiki ni wale wanosoma
Kiswahili na hata wale wenye mapenzi ya lugha ya Kiswahili pia wanaweza
kujiunga na chama hiki.
Chama hiki kina utaratibu wa kuandaa makongamano ambapo
wanachama wake kutoka nchi zote za Afrika Mashariki hupata fursa ya kukutana
mara moja kila mwaka. Pamoja na utaratibu wa chama kuandaa makongamano pia
uanzishwaji wake umeambatana na malengo kadhaa ambayo ndiyo dira inayoiongoza
chama kwa mujibu wa katiba, malengo hayo ni haya yafuatayo:
1.
Kuwapa wanachama nafasi
ya kujadili, kuimarisha, kuendeleza na kukuza vipawa vyao vya lugha na fasihi
ya Kiswahili.
2.
Kuamsha ari ya mapinduzi
ya utamaduni wa lugha ya kiswahili.
3.
Kueneza lugha ya
kiswahili ndani na nje ya nchi.
4.
Kushirikiana na vyama
vingine katika juhudi za kuendeleza na kuimarisha lugha ya kiswahili ndani na
nje ya nchi wanachama.
5.
Kuwaunganisha wanafunzi
wa kiswahili Afrika Mashariki na kati katika kukikuza kiswahili.
6.
Kushirikiana na asasi
mbalimbali zinazojihusisha na ukuzaji na uenezaji wa kiswahili ndani na nje ya
nchi kama vile BAKITA, TATAKI, TAKILUKI, UWAVITA, CHAKAMA, BAKIZA n.k.
7.
Kuchapisha kijarida cha
chama na machapisho mengine ili kusaidia kueneza taaluma ya kiswahili.
8.
Kuweka kumbukumbu ya
wataalamu wa kiswahili kwa nia ya kuwatumia katika kufanikisha malengo ya chama
na wadau wa Kiswahili.
9.
Kuratibu makongamano na
mijadala mbalimbali inayohusiana na taaluma ya kiswahili.
Pamoja na malengo hayo, lengo kuu la chama hiki ni kueneza
Kiswahili lakini sasa wanakienezaje? Wanachama wa chama hiki ambao ni nchi wanachama
wa jumuia ya Afrika mashariki wanakawaida ya kuandaa makongamano kwa ngazi ya
kitaifa na ngazi ya kimataifa.
Kwa ngazi ya kitaifa kila nchi huandaa kongamano kila mwaka
ambalo linawakutanisha wanachama wote kutoka vyuo mbalimbali katika nchi husika.
Katika kongamano hilo mada mbalimbali zinazohusu lugha ya Kiswahili na
mustakabali wake hujadiliwa lakini pia maazimio mbalimbali huchukuliwa juu ya
maendeleo ya chama. Sasa katika mijadala kama hii inatoa nafasi ya Kiswahili
kukua kwani makala mbalimbali huandikwa ambazo pia husomwa na watu mbalimbali.
Makala hizi pia zimekuwa zikichapishwa katika majarida ya chuo husika na pia
zimekua zikichapishwa mtandaoni ambapo hutoa fursa kubwa kwa watu wengi zaidi
kuzifikia na kusoma, hivyo kwa njia hiyo Kiswahili kinakua kimeenea.
Dhima
ya kila Asasi inayokuza Kiswahili
Elezea dhima ya kila asasi inayokuza Kiswahili
Mafanikio na Changamoto Zinazovikabili Vyombo vya Ukuzaji wa
Kiswahili
Mafanikio
·
Vyombo vya ukuzaji wa
Kiswahili vimejitahidi sana kukuza lugha ya Kiswahili, kwa hali ya Kiswahili
ilivyo sasa ni matokeo ya juhudi za vyombo hivyo. Mafanikio ya vyombo hivyo ni
pamoja na haya yafuatayo:
·
Machapisho ya lugha ya
Kiswahili ni mengi sana nchini na nje ya nchi, kufanya mafunzo ya Kiswahili,
kukua kwa matumizi ya Kiswahili na kuongezeka kwa idadi ya watumiaji wa
Kiswahili nchini.
·
Matumizi ya lugha ya
Kiswahili katika sehemu rasmi hasa katika ofisi za serikali na ofisi za watu
binafsi inadhihirisha mafanikio ya jitihada za vyombo hivi kuhimiza matumizi ya
lugha ya Kiswahili.
·
Kufundshwa kwa lugha ya
Kiswahili kama taaluma kwa ngazi ya shahada ya awali, uzamili na uzamivu. Hizi
ni jitihada za TATAKI katika kuhakikisha kunapatikana wataalamu wa lugha ya
Kiswahili, hivi sasa TATAKI wanafundisha lugha ya Kiswahili kwa ngazi ya
shahada ya awali, uzamili na uzamivu.
·
Matumizi ya lugha ya
Kiswahili katika vyombo mabalimbali vya kimataifa, matumizi ya lugha ya
Kiswahili katika vikao vya Umoja wa Afrika na pia ufundishwaji wa lugha ya
Kiswahili katika vyo mabalimbali Duniani ni ishara tosha ya kuonesha mafanikio
ya jitihada za vyombo vya ukuzaji na uenezaji wa Kiswahili.
Changamoto
·
Vyombo hivi vinakabiliwa
na upungufu wa wataalam. Wataalamu wengi waliobobea katika taaluma za Kiswahili
wanakimbilia nje ya nchi wakidhani huko ndiko kuna maslahi mazuri zaidi.
·
Upungufu wa fedha za
kuendeshea shughuli za ukuzaji wa Kiswahili katika vyombo hivi pia limekuwa ni
tatizo sugu. Kwa hiyo shughuli za ukuzaji wa Kiswahili zinakuwa zinakwenda taratibu.
·
Taasisi hizi pia
zinashindwa kujitangaza vizuri kutokana na kwamba hazina vyombo vya habari
binafsi ambavyo vingeweza kutumika kutangaza shughuli zao. Jambo hili
limesababisha vyombo hivi kushindwa kutoa elimu ya Kiswahili kwa kutumia vyombo
vya habari kutokana na kwamba gharama za kufanya hivyo ni kubwa.
·
Vyombo hivi baadhi havina
ofisi za kudumu, na hivyo kuhamahama jambo ambalo linaathiri utendaji kazi wa
vyombo hivyo.
No comments:
Post a Comment