Wednesday, December 4, 2019

Uhakiki fani katika tamthiliya ya Orodha

Fani katika Tamthiliya ya Orodha
Hakiki fani katika tamthiliya ya Orodha
JINA LA KITABU
Jina la kitabu ORODHA ni sadifu kwa yaliyomo. Katika kitabu inatajwa orodha ya mambo ambayo yanaweza kusaidia kuepusha UKIMWI. Orodha hii inatolewa na mhusika Furaha ambaye aliomba isomwe katika mazishi yake. Mambo hayo au orodha hiyo ni pamoja na uwazi, ukweli, uadilifu, matumizi ya kondom, uelewa, upendo, elimu, uwajibikaji na msamaha. Mwandishi anaona kuwa endapo mambo haya yatazingatiwa hakika tutapunguza maambukizi zaidi ya virusi vya UKIMWI.
UTANGULIZI
Tamthiliya ya Orodha ni tamthiliya inayohusu suala zima la ugonjwa wa UKIMWI na madhara yake katika jamii. Mwandishi anaweka wazi kuhusu gonjwa hili. Mhusika mkuu Furaha anaathirika na gonjwa hili na kufariki dunia. Kimaudhui tamthiliya hii imesawiri maisha ya sasa ya jamii ya Watanzania kwani ugonjwa huu bado ni tishio. Kwa upande wa fani, mwandishi amewaumba vyema wahusika wake, muundo wake ni unaomvutia msomaji kujua ni nini kingeendelea mbeleni, ameteua lugha nzuri ya kisanaa. Haya yote yanajielekeza katika uchambuzi tutaoenda kuufanya.
MUUNDO
Mwandishi ametumia muundo changamano kwani katika sehemu ya 1 na 2 anatuonesha mazishini ambapo yanafanyika mazishi ya Furaha. Sehemu ya 3-20 anaanza kutuelezea juu ya maisha ya Furaha mpaka kifo chake ambao huu ni msago au muundo sahili. Halafu sehemu ya 17-19 na ishirini 20 anatuonesha juu ya mzozo wa orodha na hatma ya mazishi ya Furaha.
Mwandishi ameweka kazi yake katika onyesho moja. Na katika onyesho hilo ameweka sehemu ndogondogo ishirini zinazojengana kukamilisha tamthiliya nzima.
·                     Sehemu ya kwanza:Inaanza kwa kuonesha vifani vinne vimeganda kifani cha kwanza, wahusika wameganda katika mikao inayotambulisha wasifu wa wahusika. Kifani cha pili kinaonesha wagonjwa wakiwa katika mateso. Kifani cha tatu kinaonesha wagonjwa wakiwa katika maumivu makali sana.
·                     Sehemu ya pili:Hapa inaelezwa juu ya siku ya msiba wa Furaha. Mama yake Furaha anaeleza watu kuwa Furaha aliacha orodha ambayo alitaka isomwe hadharani katika mazishi yake. Suala hili linazua mgogoro na hofu kuu kwa watu. Padre James anaweka juhudi kuzuia barua isisomwe.
·                     Sehemu ya tatu:Sehemu hii tunaoneshwa juu ya maisha ya Furaha nyumbani kwao, baba na mama yake na wadogo zake. Baba yake anaonekana kutofurahishwa na mwenendo wa Furaha kwani anamkanya kwa maneno makali ya laana. Kama vile hatopata mtu wa kumuoa. Anamuasa Furaha kuonesha mfano mzuri kwa wadogo zake.
·                     Sehemu ya nne:Hapa Furaha kwa mara ya kwanza anatoroka nyumbani kwao usiku wa manane pamoja na Mery kwenda baa. Mdogo wake anabaini kitendo hicho na kutishia kushitaki kwa wazazi lakini Furaha anamtishia kumchinja.
·                     Sehemu ya tano:Wanaonekana Mery na Furaha wako baa wakinywa pombe na kucheza na wanaume. Hapa Furaha anajifunza mambo mapya mabaya kama vile ulevi kupitia rafiki yake Mery. Pia anaanza mahusiano ya mapenzi na wanaume mfano Bw. Ecko.
·                     Sehemu ya sita:Hapa Furaha anamwendea Padre James kwa ajili ya maungamo kwani alikunywa pombe na kulala na wanaume, lakini Padre James anamwambia Furaha aende kesho yake katika chumba chake cha kujisomea nyuma ya kanisa na taa zitakuwa zimezimwa kuficha utambulisho. Na hapa ndipo Furaha anapozini na Padre kwani Padre alishikwa na tamaa.
·                     Sehemu ya saba:Baba na Mama Furaha wanamkanya Furaha kuhusu tabia yake ya umalaya na ulevi. Furaha anaomba msamaha.
·                     Sehemu ya nane:Furaha anakutana na Kitunda aendapo sokoni, katumwa na mama yake. Lakini anamkuta Kitunda akisikiliza mziki Furaha anashawishika, Kitunda anamshawishi zaidi na hata avute bangi ila hakubali. Pia wanazungumzia juu ya jiji la Dar es Salaam. Habari hizo zinampagawisha Furaha na kutamani sana aende.
·                     Sehemu ya tisa:Salim anarudi toka masomoni Dar es Salaam. Anaonana na mpenzi wake wa zamani Furaha. Wanasalimiana kwa hamu na furaha tele.
·                     Sehemu ya kumi:Salim na Furaha wanakutana na kuelezana habari za kitambo kwani walitengana kwa muda mrefu, wanapanga mipango juu ya mahusiano yao.
·                     Sehemu ya kumi na moja:Wanakijiji wanazungumzia juu ya tabia ya umalaya ya Furaha, pia wanazungumzia juu ya mahusiano ya Furaha na Salim. Hawapendezwi na tabia ya Furaha na kuamua kumtaarifu mama yake.
·                     Sehemu ya kumi na mbili:Mama Furaha anachukua jukumu la kumhoji mwanae juu ya tabia yake. Furaha hakubaliani na lolote. Hali ya Furaha inaanza kudhoofu na mama yake anaaingiwa hofu.
·                     Sehemu ya kumi na tatu:Furaha yupo sebuleni akisali. Baba yake anamuonya zaidi na kumshauri aolewe na Salim kwani ni kijana mzuri anayefaa.
·                     Sehemu ya kumi na nne:Hapa hali ya Furaha inazidi kutetereka, anachukuliwa vipimo vya damu na kugundulika kuwa ana virusi vya UKIMWI. Hali hii inamshitua sana mama yake. Anamuhoji kama aliwahi kutembea na mwanaume yeyote, anamueleza njia za upataji wa UKIMWI na Furaha naanza kulia kwa kutambua kosa lake.
·                     Sehemu ya kumi na tano:Wanakijiji wanapata habari juu ya kuumwa kwa Furaha na wanazieneza. Juma, Kitunda, Padre James, Salim, Bw. Ecko wanapata pia habari hizi. Wanaingiwa na hofu kubwa endapo watakuwa wameambukizwa UKIMWI au majina yao yamo kwenye orodha?
·                     Sehemu ya kumi na sita:Salim anaamua kumtembelea Furaha nyumbani. Akiwa katika hali mbaya sana ya ugonjwa Furaha anamuweka wazi Salim juu ya kuathirika kwake kwa UKIMWI. Salim anaingiwa hofu anamuomba Furaha barua yenye orodha kwa shauku lakini hampatii. Hali hii inamuudhi Salim. Na hapa ndipo Furaha anapokata roho!
·                     Sehemu ya kumi na saba:Hapa tunaelezwa juu ya juhudi za Bw. Ecko, na Juma za kutaka kuiba barua yenye orodha katika chumba alicholazwa maiti ya Furaha. Lakini hawafanikiwi. Familia ya Furaha wanaamini kuwa kuna mizimu katika chumba cha maiti kutokana na kelele za Juma na Bw. Ecko, na Kitunda.
·                     Sehemu ya kumi na nane:Padre James anaomba kusomewa barua hiyo kabla ya mazishi lakini mama furaha anakataa. Anaamua kuitafuta mwenyewe sebuleni bila mafanikio.
·                     Sehemu ya kumi na tisa:Asubuhi siku ya mazishi. Ecko, Juma na Salim wanaonekana wakitafuta suluhu ya namna ya kuzuia orodha isisomwe ila hawafanikiwi.
·                     Sehemu ya ishirini:Ni siku ya mazishi ambapo Mama Furaha anaisoma barua ya orodha. Padre James anajitahidi kumpinga mama Furaha asiisome orodha lakini hafanikiwi. Salim anapora barua na kuchana baadhi ya sehemu lakini hiyo haiharibu kitu kwani anaunga vipande na kusoma mbele ya wanakijiji wote. Ndani ya orodha hakuna jina la mtu yeyote lililotajwa bali mambo yatakayosaidia kuuepuka UKIMWI.
MTINDO
Mtindo aliotumia mwandishi ni wa dayalojia au majibizano. Mwandishi ameunda visa na masimulizi yake kupitia majibizano ya wahusika. Pia kwa kiasi kidogo ametumia mtindo wa monolojia, mfano uk. 27 padre James anasema:
“Bwana natazamiwa kuiendesha sala hiyo! Ni kitu ambacho hakikubaliki! Shetani yu kazini kjijini hapa! Furaha anavuna mbegu ya kifo aliyoipanda! Oh! Njia ya mtumishi wa bwana ni ngumu. Imejaa majaribu! Mtu lazima awe na nguvu na kuileta kazi ya bwana kwa watu hawa wa kawaida. Nimepewa kazi iliyo rahisi lakini ni ngumu sana! ni kazi ya upweke!!! Mwili ni mdhoofu! Oh Bwana utulinde.”
Hapa padre James aliongea mwenyewe akifikiri kuwaza na kujutia kazi anayofanya. Pia uk. Huohuo tunaona maneno ya Salim anaongea mwenyewe, pia uk.10, 23,37 na 40.
Pia mwandishi ametumia mtindo wa barua katika kazi yake lengo ikiwa ni kuweka mkazo katika mambo muhimu ya kuzingatia ili kuiepuka UKIMWI. Barua yenyewe ilisema hivi, uk.44“Kwa Kijiji changu kipendwa,
Nawasukuru kwa kufika kwenu na kuyasikiliza maneno yangu ya mwisho. Msiogope kwani nadhani maneno haya yanaweza kuwasaidia. Katika hii miezi ya mwisho nimelala kitandani nikifa, nikizidi kuugua. Nilipata muda mwingi wa kufikiri, kubadilika kukua kama mtu; hata ninapokuwa nakufa. Katika ukurasa unaofuata kuna Orodha ya vitu amabvyo vilisaidia kuyafupisha maisha yangu, orodha ambayo inaonesha kwenu nyote ukweli juu ya kifo changu. Mama, tafadhali wasomee watu wote orodha hii.
·                     Uepukaji
·                     Kondomu,
·                     uaminifu ,
·                     elimu,
·                     welewa,
·                     uwazi,
·                     uadilifu,
·                     uwajibikaji,
·                     ukweli,
·                     upendo,
·                     msamaha.
Ukosefu wa mambo yote haya ndio ulioniua. Ufuatiliaji wa mambo yote haya unaweza kuwaokoa ninyi nyote. Chukueni orodha yangu na muinakili. Ipelekeni kwenye vijiji vingine, miji mingine na majiji mengine katika nchi yetu hii nzuri. Wanusuruni watu wetu ili waweze kuyafaidia maisha kikamilifu .Wanusuruni watoto wetu ili wasiwe yatima. Muinusuru Afrika…. Afrika yetu nzuri
Kwa kijiji changu kiishi maisha marefu na kiwe na furaha! Msihukukumu mapema mno. Kwa Mama, baba dada zangu, nawapenda. Jaribuni kuwa wenye furaha wakati mnaweza kufanya hivyo.Wenu awapendae Furaha.”
Matumizi ya nafsi
Mwandishi ametumia nafsi mbalimbali na hii ni mifano:
·                     Nafsi ya kwanza umoja na wingi:Uk.28 Salim: “nilidhani sitakuona tena sijakuona muda mrefu”Uk.42 “oh huwezi kuamini jinsi tulivyojaribu”.
·                     Nafsi ya pili:Salim : usifurahi kupita kiasiSalim: hufai kuhukumu unalala kama…..Mama Furaha: usiwe hivyo wewe u mtoto mzuri.
·                     Nafsi ya tatu:Mama Furaha: kabla Furaha hajafa alitaka niahidi kumfanyia kitu fulani hapa kwenye mazishi ingawaje alikuwa na maumivu na mateso aliandika barua hii hapa na kunipa.
MATUMIZI YA LUGHA
Lugha aliyotumia mwandishi ni lugha fasaha na inayoleweka kwa wasomaji wake.
Matumizi ya tamathali za semi
·                     Sitiari:Uk.2 “Waridi changa” “Ua kavu” –Mama anamfananisha Furaha na waridi au ua.Uk.4 “Nyie Mbu mlolaaniwa” –Baba Furaha anawaita wadogo zake Furaha;Uk.6 “Ua” –Furaha.Uk.25 “Slim”- UKIMWI. Wanakijiji wanaufananisha ugonjwa huu na jina hili kutokana na sifa yake ya kukondesha mwili.
·                     Tashibiha:Uk.18 “yeye ni kama Punda wa kijiji”.Mwanakijiji wa 1 anamfananisha Furaha na Punda kutokana na tabia yake ya kuwa na wanume wengi. Malaya.Uk.13. “kisura ni kama jiji la New York…”Uk.43 “…vipande vinaanguka kama theluji”.
·                     Mubaalagha:Uk.13 “kisura ni kama Jiji la New York ya Afrika Mashariki. Kule kuna majengoMajengo makubwa kiasi kwamba unaweza kuona mlima Kilimanjaro kwaJuu” pia anasema“Ndiyo mpenzi na Maduka… wana moja linaloitwaShoppers Plaza…! Pengine ndilo eneo kubwa lenye maduka makubwaKuliko yote katika Afrika”Uk.20 Furaha: nani aliyesema mambo hayo?Mama Furaha: Nusu ya kijiji kizima badala ya watu wengi. Mama Furahaanazidisha chumvi Kuonesha ukubwa wa hilo jambo.
·                     Tafsida:Uk.7 maongezi kati ya wahusika;Mary: hiyo ni bia yake ya mwanzo.Furaha: ni chunguMary: ladha yake utaizoea tuBw. Juma: kama ulivyizoea wewe mayai yangu madogo!Bw. Ecko: Unaona! Inashangaza jinsi ambavyo mtu unaizoea haraka ladha hiyo!Bw. Juma:(kwa mary) kama ulivyofaanya wewe, mishikaki yangu midogo….Mazungumzo haya yamepunguza ukali wa maneno, maneno kama vile “Mishikaki” na “Mayai” ni sehemu za siri.
Mbinu nyingine za kisanaa
·                     Mdokezo:Uk.8 “ndiyo padre….. ni …..”Uk.9 “Furaha…..fur….tuta…..”Uk.20 “ame…..tuseme…..”Uk.36 “misamaha padre mi…”Uk.44 “uepukaji….”
·                     Nidaa:Uk.15 “Ooo!”Uk.34 “Oh!”Uk.41 “Eee”
·                     Takriri:Uk.28 “Hapana hapana hapana nitauona!” “mpumbavu mpumbavu mimi”Uk.9 “hili ni jambo zito sana… sanasana…..sana hasa…”Uk 44 na 45 maneno haya yamerudiwa kuonesha msisitizo.Mwanakijiji wa 2: kondomMwanakijiji wa 3: elimuMwanakijiji wa 4: elimuMwanakijiji wa 1: uwaziKitunda: uadilifuPadre James: ukweliMary: upendoSalim: msamaha.
·                     Tashtiti:Uk.20 mama Furaha: wewe na marafiki zako wa kiumeFuraha: marafiki gani wa kiume?Furaha anauliza swali ambalo majibu yake anayo ila tu anataka kuupindisha ukweli.Uk.38 baba: msalaba wako, padri. Uko shingoni mwako!Padre James: kweli?Baba: padre!Padre James: hakika?Padre James alijua wazi kuwa msalaba ulikuwa shingoni lakini kutokana na kutaka kuuficha ukweli alipokutwa katika pilika za kutafuta barua na kusingizia amedondosha msalaba. Alijifanya kuuliza kama vile hajui.
·                     Onomatopea au tanakali sauti:Uk.33-34 “Myaau!” Uk.35 “Oooowww!”
Matumizi ya semi
·                     Misemo:Uk.27 “Furaha anavuna mbegu ya kifo aliyopanda”
WAHUSIKA
FURAHA
·                     Ni binti mdogo wa miaka kati ya 13-19
·                     Ni Malaya
·                     Anaathirika kwa ugonjwa wa UKIMWI
·                     Alikuwa na bidii na mwenye kujituma
·                     Ana tama
·                     Ni mlevi
·                     Ni mkweli na muwazi
·                     Ni jasiri
BABA
·                     Ni baba yake Furaha
·                     Ni mkali
·                     Ana upendo
MAMA FURAHA
·                     Ni mama yake Furaha
·                     Ni mkweli na muwazi
·                     Ana upendo
·                     Ni jasiri
·                     Ni mchapakazi
·                     Ni mpole
·                     Ana msimamo
·                     Anafaa kuigwa na jami
MARY
·                     Ni binti mdogo
·                     Ni Malaya
·                     Si rafiki mwema
·                     Anachangia kuharibu maisha ya Furaha
·                     Ni mlevi
·                     Anapenda anasa
·                     Ana tama
·                     Hafai kuigwa na jamii
·                      
BW. ECKO
·                     Ni mwanaume mtu mzima
·                     Ni Malaya
·                     Si muaminifu katika ndoa yake
·                     Ni mrubinifu kwa mabinti wadogo
·                     Ni mlevi
·                     Ni mfanyabiashara
·                     Ni muathirika wa UKIMWI
JUMA
·                     Ni mwanaume mtu mzima
·                     Ni Malaya
·                     Ni laghai kwa mabinti wadogo
·                     Ni mlevi
·                     Anapenda anasa
·                     Ana tama
·                     Ni rafiki wa Bw. Ecko
PADRI JAMES
·                     Ni mtumishi wa Mungu katika kanisa katoliki
·                     Si muadilifu
·                     Anaogopa ukweli na uwazi
·                     Ni dhaifu kwa wanawake
·                     Anaweza kuwa ni muathirika wa UKIMWI
KITUNDA
·                     Ni kijana wa mtaani
·                     Anapenda anasa
·                     Ana tama
·                     Ni mlaghai kwa wasichana
·                     Ni muhuni
·                     Ni mlevi na mvuta bangi
·                     Ana lugha ya kihuni
SALIM
·                     Ni kijana wa kiume
·                     Ni msomi
·                     Ni mchumba wa Furaha
·                     Anaweza kuwa ni muathirika wa UKIMWI
·                     Si mkweli na muwazi
·                     Si muadilifu
·                     Wanakijiji 1,2 na 3
·                     Ni wanakijiji katika kijiji cha Furaha
·                     Hawana elimu juu ya UKIMWI
·                     Ni wambea
·                     Wana imani potofu
DADA MDOGO
·                     Ni mdogo wake Furaha
·                     Ana tabia njema
·                     Ni mkweli lakini muoga
·                     Hapendezwi na tabia ya dada yake
MANDHARI

Mandhari aliyotumia mwandishi ni ya vijiji vya Afrika Mashariki kwa ujumla wake. Mwandishi ametumia mandhari hii makusudi kwani imeendana na yale anayoyazungumza katika kitabu. Suala la ujinga na upotofu wa dhana kuhusu UKIMWI lipo zaidi vijijini. Wanakijiji hawaelewi juu ya UKIMWI. Mambo anayoyaibua mwandishi yanaendana na jamii ya watu wa vijiji hivyo mandhari ni sadifu.

No comments:

Post a Comment

CHUO CHA UALIMU MONTESSORI-MTWARA

Uhakiki Fani katika Ushairi wa Malenga Wapya

Fani katika Ushairi wa Malenga Wapya Hakiki Fani katika Ushairi wa Malenga Wapya MWANDISHI: TAASISI YA KISWAHILI, ZANZIBAR WACHAPISHA...